Akizungumza katika mkutano wa Kamisheni Usalama wa Kitaifa ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) jana Jumanne, Meja Jenerali Mousavi aliwasilisha arifa kuhusu hali ya sasa na utayarifu wa kujihami wa wanajeshi mkabala wa tishio tarajiwa la maadui.
Msemaji wa tume hiyo, Ebrahim Rezaei, aliwasilisha matamshi ya Mousavi, akisema kuwa Vikosi vya Jeshi la Iran vimejiandaa kikamilifu na vipo katika kiwango cha juu cha utayarifu wa kulilinda taifa na kuingia kwenye vita vya kujibu chokochoko.
"Wako tayari kutoa jibu la kujutisha kwa kitendo chochote cha uchokozi. Ikiwa uchokozi wowote utatokea dhidi ya nchi yetu, jibu letu litakuwa madhubuti na la uchungu zaidi kuliko hapo awali. Utayarifu wetu sasa ni mkubwa kuliko ilivyokuwa miezi mitatu iliyopita," Rezaei amesema, akinukuu kauli ya Mousavi, Mkuu wa Kamandi ya Majeshi ya Iran.
Wajumbe wa Kamisheni ya Usalama wa Kitaifa na Sera ya Nje ya Bunge la Iran wamepongeza juhudi zisizo na kikomo za wanajeshi wa Jamhuri ya Kiislamu katika kulilinda taifa, na kusisitiza uungaji mkono wao kamili kwa vikosi hivyo. Kamanda huyo mwandamizi wa jeshi la Iran amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ilishinda katika vita vya siku 12 vya kichokozi vilivyoanzishwa na Marekani na utawala wa Israel mwezi Juni, na ilifanikiwa kumlazimisha adui asalimu amri.
Meja Jenerali Mousavi amesisitiza kuwa, vikosi vya jeshi la Iran vitatoa jibu la kukandamiza, la kujutisha na la maumivu zaidi kwa uchokozi wowote unaoweza kufanywa na Utawala wa Kizayuni wa Israel na Marekani.
Your Comment